Sunday, January 17, 2010

Buibui la kizanzibari


Wanawake wa Kizanzibari na mabuibui


Buibui linasafari refu kutoka huko lilikotoka huko kwao Iran, lilikuwa na lengo moja tu nalo ni kustiri, na ahadi hiyo ninanvyoona mimi inaitekeleza, ikiwa mwanamke analolivaa anahishima au laa, halijali kazi yake kubwa ni kumstiri mvaaji na kumpa heshma. Kabla ya buibui hili la kamba, hapa Zanzibar pakivaliwa buibui la lembwani, ni guo refu la silk, wakivaa wanawake wenye uwezo tu, tena wakijifunika gubi gubi, hasa wanawake wa kishirazi walokuwa na uwezo, likivaliwa sana pande za Hurumzi, ama lilipotea baada ya kuingia barkowa, wanawake wengi wakiiga Waarabu Kutoka Oman, Kuweit, Baharein n.k.
Wazanzibari walirudisha tena mtindo wa kuvaa tena buibui, lakini mara hii lilikuwa la kamba, kulikuwa na mabadiliko ya vitambaa sana vikitumika vya thamanini, na yakapatikana mabuibui ya thamanini, ya ogri, ya mende, ya lozi, ya kaniki, ya ukoko wa haluwa, ya mauwa, ya kitina na la bati ambalo likilia kama bati ukitembea linatowa sauti, la ogri ni laini sana, la ukoko wa haluwa kitambaa chake kinakuwa kama kina povu, na mende lilikuwa ukilishika lina madudedude,   muuuzaji wake mkubwa alikuwa Gamia alikuwa na duka karibu na Saleh Madawa karibu na kwa Uncle.
Uvaaji wa mabuibui ya kamba ulishamiri sana wakati wa vita kuu ya kwanza, buibui ambalo linaloshonwa ilikuwa muhimu liwe na kamba ya kulifungia, ukaya ambao unaoshuka ncha mbili ima unakuwa mrefu au mfupi inategemea, ikiwa unataka ujifunike gubi gubi au unataka kuliachia au ulitie zoro, mtindo ulokuwa marufu sana hapo zamani, uliopata jina baada ya kuja mchezo wa zorro, Johnston Meculley alitunga kitabu [novel] kilichoitwa The Mark of Zorro, ambapo mwaka 1937 iliektiwa sinema yake, huko Amerika ‘Rides Again’, na kufikia mwaka 1940 kwa vile watu wa Zanzibar waliiona filamu hiyo, waliupa uvaaji wa buibui kujifunika kuonekana macho tu jina hilo la Kizorro, wari wakipendelea kuchungulia maharusi kwa mtindo huu, kwa vile zamani ilikuwa aibu kwao kwenda maharusini. Mtindo wa kuvaa ninja pia umeigwa jina  kwenye sinema, Ninja I na Ninja II, baada ya kuja tu filamu yake, na hii inaonyesha wazi vipi tunaweza kuathirika nazo. Uvaaji wa buibui baadae ulibadilika kutokana na mazingira, kwa mfano bi Nunu kwa vile yeye alikuwa ni mke wa sultani ilimbidi alipunguze buibui kwa chini ili aweze kupanda vizuri vyombo kama meli, boti, gari n.k na wanawake wengi wakanza kuiga, kwa hiyo harakati zilibadilisha uvaaji wa mabuibui, Kama kuna mtindo unaoitwa kibiriti ngoma, mtindo wa kulipandisha buibui kuliweka shingoni, mtu akikuona umefanya hivyo anajuwa hakuna salama, umefikwa na jambo, mtindo ulopata jina kituo cha polisi cha kibiriti ngoma hapo Ng’ambo polisi. Kwa hivyo ushonaji wa buibui la kamba lilizingatia mambo mengi, ima unaweza kujistiri au ikibidi unaliachia watu waione [wanawake wenzao] umevaa nguo gani, inategemea mazingira. 



Seyyid Kalifa na Bi Nour


Cha kukitisha kuwa vijana hawalipendi buibui la kamba, wanafurahishwa na abaya, ambalo haliwezi kubadilika badilika kimazingira, na pia hata halikidhi mahitaji ya mwanamke, hawezi kuonyesha uzuri wa nguo yake akiwa yuko pamoja na wanawake wenzake. Buibui la asili hufuliwa kwa harita, huanikwa kwa ustadi na hukunjwa kwa ma-ain. Baada ya kufukizwa na kutiwa maal-uud.

No comments:

Post a Comment